Wednesday, September 3, 2008

KESI YA ZOMBE!!

Leo ni jumatano, septemba 3 2008,
Siku ya 247 tangu mwaka kuanza, zimebaki siku 119 kuumaliza mwaka 2008. Chungu cha pili Ramadhan 1429 Hijria.

Baadhi ya watu waliandamana na msafara wa Mahakama kuu, ilipohamia katika msitu wa Pande kujionea eneo ambalo wafanyabiashara wasio na hatia waliuawa na polisi kwa kudaiwa kuwa ni majambazi.

Mabishano makali yalizuka jana katika Msitu wa Pande Mbezi Louis, kati ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (ACP) Abdallah Zombe na mshtakiwa wa 11 Koplo Rashidi Lema, wakati Mahakama Kuu ilipohamia katika msitu huo kuona eneo linalodaiwa kuwa wafanyabiashara wa madini wa Mahenge na dereva teksi waliodaiwa kuwa majambazi waliuawa huko.

Mabishano hayo yalitokea muda mfupi baada ya mahakama kukamilisha shughuli zake katika eneo hilo, wakati watu walipoanza kuingia katika magari yao wakiwemo washtakiwa ili kuendelea na msafara, kisha Zombe alisikika akisema kuwa hajawahi kufika katika msitu huo.
“Walahi wabilahi sijawahi kufika huku mambo haya makubwa kumbe mji huu ni mkubwa namna hii!” alisikika Zombe.

Baada ya kutoa kauli hiyo, mshtakiwa wa 11 Koplo Rashid naye alisikika akimjibu Zombe kwa hasira.“Hilo utaeleza mahakamani na utaeleza sehemu mliyokuwa mnanywea bia siku ile na bia zilinyweka ngapi,” alisema Rashid.Koplo Rashidi ndiye aliyeeleza kuwa majambazi yanayodaiwa kuuawa na polisi yaliuawa katika Msitu wa Pande na si eneo la Sinza C kama polisi walivyodai.

Mahakama ilianzia msafara wake katika eneo la Sinza C, ambalo linadaiwa na polisi kuwa majambazi hayo yalikamatwa eneo hilo.Katika eneo hilo la Sinza kabla mahakama haijaondoka, Jaji Kiongozi Salum Massati aliwauliza washitakiwa kama walikuwa na lolote la kuzungumza lakini walijibu kuwa hawakuwa na lolote.

Katika eneo la ukuta wa Shirika la Posta kunakodaiwa kuwa na matundu yaliyotokana na mapambano ya polisi na majambazi, Zombe aliiomba mahakama itafute mtu ambaye atapewa bunduki na kupiga katika ukuta huo ili kubaini ukweli wa matundu hayo.Jaji alimjibu Zombe kuwa suala hilo litazungumziwa mahakamani.

Baadhi ya mahojiano baina ya wakili wa serikali Alexander Mazikila na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Edson Mmari, ambaye ni shahidi wa 30 katika kesi hiyo yalikuwa kama ifuatavyo.
Wakili Mzikila: Je, mlipofika hapa (Sinza) waliwaeleza ni magari gani ya polisi yalikuja?
Shahidi: Walisema lilikuja gari la Bageni (mshtakiwa wa pili) na gari la Makele (Mshtakiwa wa tatu).

Wakili: Waliwaeleza baada ya kuwakamata marehemu walielekea njia ipi?
Shahidi: Walielekea njia ya upande wa magharibi.
Wakili: Wakati majambazi hayo yanakamatwa waliwaeleza wao walikuwa wapi?
Shahidi: Walikuwa eneo la Maduka.
Wakili: Baada ya kutoka eneo la Sinza C mlielekea wapi?
Shahidi: Tulienda Sam Nujoma kwenye eneo ambalo fedha za kampuni ya Bidco ziliporwa.
Wakili: Je, fedha hizo zilikuwa zimebebwa kwenye gari gani?
Shahidi: Zilibebwa kwenye gari aina ya Mercedes Benz la Kampuni ya Bidco.
Wakili: Katika eneo hili (Sam Nujoma) kuna mabadiliko yametokea, je, kitu gani kimekufanya ulikumbuke, uliweka alama?
Shahidi: Nimelikumbuka kwa sababu upande wa pili wa barabara kulikuwa na Banda la Kampuni ya Konoike.
Wakili: Baada ya kutoka hapa mlielekea wapi?
Shahidi: Tulielekea katika eneo la ukuta wa Posta mahali ambako kunadaiwa kulikuwa na matundu ya risasi yaliyotokea baada ya majibizano ya polisi na majambazi.
Wakili: Wewe ni askari wa siku nyingi na pia ni mpelelezi unazungumziaje matundu haya?
Shahidi: Hata kama ungepiga kwa karibu na risasi ikapita kwenye mwili wa binadamu lazima ingepasua ukuta zaidi.
Wakili: Kwa kuwa Bageni aliwaeleza baada ya mapambano yale kulikuwa na majeruhi, je, nyie katika uchunguzi wenu mlibaini nini?
Shahidi: Kulikuwa hakuna majeruhi.
Wakili: Je, mliangalia kama kulikuwa na kitu kingine chochote kilichoashiria mapambano?
Shahidi: Tuliangalia ukuta wa pili lakini hatukuweza kuona kama kulikuwa na matundu ya risasi.
Wakili: Baada ya hapa mlielekea wapi?
Shahidi: Tulielekea Msitu wa Pande ulioko Mbezi Louis kwenye eneo ambalo wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliuliwa kule.
Wakili: Je, mlipofika hapa (msituni) mlizikuta maiti za hao majambazi?
Shahidi: Hatukuzikuta lakini tuliambiwa walizichukua na kuzipeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakili Majura Magafu: Je, baada ya kuonyeshwa hili eneo mliweka alama yoyote?
Shahidi: Hakuna alama maalum tuliyoweka.
Wakili: Bunju mlienda lini?
Shahidi: Siku hiyo hiyo.
Wakili: Mlipofikia hapa (Bunju) mlifanikiwa kupata nini?
Shahidi: Hatukupata kitu zaidi ya kupiga picha za kawaida za video.
Wakili: Je, picha hizo zilipigwa na nani?
Shahidi: Sajent Elly alipiga picha za video na Sajent Moja alipiga picha za kawaida.

kwa ufupi, mambo yalukuwa hivyo. Kesi hiyo inaendelea kwa wiki nzima.
Haki!!
Thomas!!!

Monday, September 1, 2008

Miaka 44, Bravo JWTZ.

Thomas Mushi
Dar es salaam September 1 2008 JWTZ………..
Jeshi la wananchi wa Tanzania limeadhimisha miaka 44 tangu kuanzishwa kwake kwa kuahidi kuendelea kutekeleza kwa vitendo madhumuni ya kuundwa kwa jeshi hilo likiwemo jukumu la ulinzi wa nchi na utoaji wa huduma kwa raia wakati wa dharura.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na waziri wa ulinzi wa Comoro Mohamed Bacar Dosar na Mkuu wa Majeshi wa Comoro Brigedia Jenerali Salimoo Mohamed ambao wamelikushukuru jeshi la wananchi wa Tanzania kwa kufanikisha kumuondoa madarakani kiongozi muasi Kanali Mohamed Bacar katika operesheni ya kijeshi visiwani Anjouan.

Viongozi hao pia walitoa mkono wa pole kwa wajane wa askari wawili wa Tanzania waliofariki dunia nchini Comoro. Askari hao ni Coplo Rafael Sarakikya kutoka Arumeru Arusha aliekufa maji siku mbili kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo wakati PRIVATE Hamis Makame kutoka kaskazini Unguja alifariki dunia kwa kuugua siku chache baada ya kumalizika kwa opesheni hiyo.

Akizungumza katika hafla fupi Makao makuu ya jeshi upanga jijini Dsm, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dr Hussein Mwinyi amesema,jeshi la wananchi wa Tanzania linajivunia rekodi yake ya mafanikio makubwa katika operesheni zake wakat wa amani na zile za kivita ambazo zimeiuletea nchi heshima kubwa

Akizungumzia hoja ya kuwataka askari wa jeshi hilo kulipa nauli katika vyombo vya usafiri, waziri Mwinyi amesema, chombo chenye maamuzi ya kutangaza agizo hilo ni Sumatra, baada ya kufanya mashauriano na wadau. Ameongeza kuwa, kufuatia ukimya wa Sumatra katika suala hilo, ni wazi kuwa bado majadiliano hayakamilika hivyo watoa huduma wasubiri agizo la Sumatra na si vinginevyo.

Kuhusu mafanikio makubwa ya opesheni Democracy Comoro iliyofuatiwa na ahadi ya Rais kuwapa nishani askari walioshiriki,mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Jenerali Mwamunyange amesema, nishani hizo zinaandaliwa na zitakapokuwa tayari umma utajulishwa.

Katika vuwanja vya Jeshi, Mkuu wa majeshi jenerali Davis Mwamunyange na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Abdurahman Shimbo wamewaongoza maafisa, askari na wananchi katika sherehe hizo ambapo wimbo mpya wa jeshi ulizinduliwa rasmi baada ya mchakato mkali uliosimamiwa na wataalamu

End……..