Thursday, August 28, 2008

KARIBUNI WASOMI UDSM

Siku chache zijazo, Chuo Kikuu cha Dar es salaam kitaanza rasmi muhula wa kwanza wa masomo kwa mwaka 2008/2009. Ni kipindi kingine chenye ratiba ndefu na ngumu ki utekelezaji hasa kwa kuzingatia majukumu ya ki taaluma yaliyopo mbele ya wanafunzi na waalimu wao.

Ni kipindi ambacho wanafunzi wapya wanaanza kuzishuhudia hekaheka za kujipatia elimu katika asasi hiyo yenye hadhi ya juu kabisa ki taaluma hapa nchini. Kila mmoja bila shaka atakuwa akimshukuru Mola wake kwa kumpa nafasi hiyo miongoni mwa ma elfu walioitaka na kuihangaikia nafasi hiyo kwa kusoma tangu mawio mpaka machweo na wakati mwingine kwa kuugeuza usiku kuwa mchana.

Wanafunzi hawa watapokelewa na wenzao wenyeji kwa furaha, wataonyeshwa mazingira na kufundishwa maana ya misamiati kibao inayotumika Chuoni ambayo ni aghalabu kwa asiye mwana chuo kujua maana yake, boom, flight, kunji, desa,kilaza, kipanga, mmbu, araivoz na mingine kibao.

Zitafanyika pia sherehe katika kumbi mbali mbali ili kuwakaribisha na hapa lazima tupeane tahadhari kwani huu huwa ni mwanzo kwa wale wasio makini kujihusisha na mambo ambayo huwa na mwisho mbaya.

Serikali kupitia bodi yake ya mikopo itawapatia fedha wanafunzi hawa ili waweze kumudu gharama za kuwepo Chuoni na kununua mahitaji muhimu. Ni vyema wanafunzi wakakumbuka kuwa makini na matumizi. Wasijisahau na kuanza kula, kunywa na kuponda raha kwani fedha wanazopata ni kidogo ukilinganisha na matumizi yake kwa muda wote watakaokua shuleni.

Ni vyema busara ikatumika katika manunuzi ya vitu vya thamani kama vile nguo, viatu, marashi ya kupendeza, simu za kisasa, redio, tv, kompyuta na vinginevyo ili kuhakikisha kuwa wanabakiwa na akiba ya kuwasogeza hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba, wengi wao hutegemea fedha hizo tu kuendeshea maisha yao muda wote wawapo Chuoni kwa kuwa hawana ndugu hapa Jijini au ndugu waliopo hawana uwezo wa kuwasaidia.

Umakini unahitajika kwa wanafunzi kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya Chakula, kulipia malazi, matibabu, nauli pamoja na kununua vifaa vya muhimu vya kufanikisha masomo kama vile vitabu.
Kutotekeleza ushauri huu kuna madhara makubwa kwani uzoefu unaonyesha kuwa, wanafunzi wasio makini huishiwa fedha zao katika kipindi kifupi kiasi cha kushindwa kununa chakula na kukosa hata nauli ya kuwafikisha Chuoni. Huu ndio mwanzo wa kufeli mitihani na mwanzo wa safari ya kurejea nyumbani wakiwa mikono mitupu.

Huu ni wakati muhimu wa kutafakari na kuanza kujenga maisha yao ya baadae kwa kuwekeza katika taaluma na kuonyesha uwezo wao binafsi wa kujisimamia na kutekeleza matarajio yao na ya familia kwa ujumla.

Kwa upande wa taaluma, wanafunzi hawa wanatakiwa kujiwekea mikakati ya ushindi. Ndoto na dua zao sasa zimetimia, yale yote waliyokuwa wakiyasikia kama hadithi sasa watayaona kwa vitendo. Kwa wale waliozoea kulala, sasa itawawia vigumu kwani masomo yanaanza saa moja kamili asubuhi na kuisha sa mbili za usiku kulingana na ratiba, ni muhimu kuhudhuria kila kipindi bila kujali umepata makazi wapi, iwe ndani ya hosteli za Chuo au Uraiani.
Hapa pia watakutana na staili mpya za kusoma, ile tabia ya kuelekezwa saana na pengine hata kutengenezewa notes itakuwa imefikia mwisho. Kazi ya waalimu huku ni kukupa mbinu na maelekezo ya kufuata ili kupata maarifa wanayoyahitaji. Hii ina maana kuwa, kukosa masomo siku moja ni sawa na kuchezea shilingi chooni.

Muda si muda itaanza mitihani ya majaribio na itafuatiwa na mitihani yenyewe, hapo Chuo huwaka moto kwa kila mwanafunzi kujaribu kila liwezekanalo ili kuendelea kubaki CHUONI kwani vinginevyo njia ya kurejea nyumbani huwa ni nyeeupeee.
Japo hakuna adhabu ya viboko kama ilivyokuwa kwa elimu ya msingi na sekondari, ni wazi kwamba upo umuhimu mkubwa wa kusoma kwa bidii na kuzingatia sheria za kitaaluma zinazowaongoza kwa muda wote wawapo Chuoni.

Miongoni mwa mambo yanayolisikitisha Taifa, Jamii na wazazi wa wanafunzi ni pale vijana hawa wanapolazimika kurejea makwao kwa kushindwa kumudu mikimkiki ya Chuo. Muda na gharama zao zote hupotea na harakati za maisha hurudi nyuma kwa kiasi kikubwa.
Ndio maana jamii inawakumbusha kuwa makini, kuzingatia masomo na kuvumilia magumu yote yatakayojitokeza katika harakati zao za kujenga maisha kwa muda wote wawapo Chuoni.
Kupata nafasi ya kujiunga na chuo ni mojawapo ya nafasi hadimu na zenye heshima kubwa kwa jamii. Jamii yote humpa heshima msomi na humtegemea kuwa mfano wa kuigwa na mchangiaji makini wa mambo ya maendeleo na pamoja na kuelekeza mbinu za kuyashinda matatizo yanayoikabili jamii.
Kutokana na ukweli huu, ni muhimu tena sana kwa wasomi hawa kujikinga na vitendo vyote vitakavyoweza kuwaondolea heshima yao mbele ya jamii.

Kutimiza maagizo yote ya kitaaluma kutawasaidia kujiepusha na vitendo viovu kama wizi wa mitihani ambao ni kosa lisilo na mjadala. Mwanafunzi makini haitaji kujenga mahusiano na mwalimu wake kwani akili yake huwa smart na humudu masomo yake kikamilifu na wakati wote migogoro ya ki taaluma humpitia mbali.

Ki afya, hakuna asiyejua habari za gonjwa baya la UKIMWI. Taarifa zisizo rasmi zinadai kuwa, wimbi la maambukizi katika taasisi za elimu ya juu nchini ni kubwa hivyo kuna haja ya kujihami na kujiepusha na tamaa ambazo ndio chanzo kikuu cha kusambaa kwa gonjwa hili miongoni mwa wanafunzi wa ngazi zote!

Kila mmoja ajitambue na kuishi kulingana na uwezo wake, kama vidole vya mkono visivyolingana ndivyo watu wanavyotofautiana ki uchumi. Wapo watoto wa vigogo na wale wa walala hoi, hawa wana maisha tofauti sana ndio maana kujitambua ni jambo la msingi litakalompa kila mmoja uhuru wa kuishi kulingana na uwezo wake.

Wanafunzi wenyeji wana wajibu muhimu wa kuwaelekeza wageni namna ya kuishi Chuoni na hawategemewi kutumia ujanja wao kwa kuwarubuni na kuwapoteza wenzao, kuwaingiza chaka kama wanavyoita wenyewe-.
Ni vyema vile vikao vya mpaka usiku wa manane kule Mabibo hostel vikaepukwa na muda huo utumike kwa kusoma. Misafara ya usiku kwenye kumbi za starehe na fukwe za bahari nayo ikawekwa kando kwani matokeo yake huwa si mema sana hasa kwa dada zetu.

Kwa kutumia takwimu za matokeo ya mitihani, kila mmoja, mgeni na mwenyeji ajifunze, aogope jinsi ambavyo mamia walivyolazimika kukiacha CHUO bila kujali walikuwa mwaka wa ngapi kutokana DISCO, sio muziki bali DISCONTINUE, neno la kiingereza linalomaanisha kuwa vita imekushinda, huwezi kuendelea na unachotakiwa kufanya ni kurejea nyumbani.

Kila mmoja akumbuke kuwa ametoka kwao peke yake na atarudi kwao peke yake, matendo yake ndio yatakayoamua hatma yake.
Ukitaka kujua uhondo wa ngoma, uingie ucheze, mi nimeingia na kuicheza, na kujua uhondo wake, ndio maana nawaasa kwa kigezo cha experience, kabla haijawa too late., wazungu wanasema, aheri mapema, the early the better, na taarifa ni nguzo muhimu ya kufanya maamuzi sahihi , ‘information is the essentential tool for better decision making’!!
Kila kheri wanafunzi woote CHUO KIKUU CHA DSM

TNM [ BA.Masscom]
4.0 GPA, Upper 2nd Honours
Udsm Ijmc
2004/2007.
Sahara Communication
Media Reporter, Star Tv/ Rfa
Dar es salaam.

2 comments:

Ndelyanarua said...

Ni mwanzo mzuri, shavu jipe mwenyewe mwana!!!!

Ndelyanarua said...

Yaaaa, kama Mary anavyoweza kuijengea heshima TBC na vitenge vyao kwa nini mimi nisiitetee FUTUHI, though huwa siitazami hata siku moja, wajomba wanabore ila ndo nifanyaje!!